
Masimulizi ya Alfu Lela U Lela, Kitabu cha 2
Mfasiri: Hassan Adam
Hiki ni Kitabu cha pili katika mfululizo wa Hadithi maarufu duniani kote za Alfu lela U Lela (au Siku Elfu Moja na Moja) zenye asili ya Arabuni na Uajemi.
Masimulizi haya ya Alfu Lela U Lela yametafsiriwa kutoka matoleo ya kiingereza na Kijerumani. Lugha hizi za Ulaya ndimo zilimotafsiriwa hadithi hizi kwa mara ya kwanza kutoka lugha za Kiajemi, Kiarabu na Kihindi.
Tafsiri ya Kiingereza ilifanywa na Sir Richard Burton ambaye anafahamika huku kwetu kama mmoja wa wageni wa kwanza kutoka Ulaya na ati "kuvumbua" sehemu zile walizofika.
Tafsiri ya kwanza ya kiswahili ilifanywa mwaka 1928 na katika kufanya hivyo sehemu nyingi zilikatwa au ziliachwa makusudi bila kuzitafsiri kwa sababu wamisionari hawakutaka wasomi wa Kiswahili wasome baadhi ya sehemu kwa sababu zao wenyewe. Matoleo haya, kwa kifupi, ndio yenye hadithi kamilifu kwa uhakika; yaani mtiririko wa visa na maana halisi ya hadithi kama zilivyotungwa na kutafsiriwa na magwiji wa lugha hizo mbili zaidi ya miaka mia moja iliyopita. Wale wasomaji waliozisoma enzi hizo watataka kuzisoma tena ili wapate uhondo wote kama zilivyotungwa asilia; na wasomaji wapya hawatakosa kujua kwa nini hadithi hizi ni hazina kwa wasomaji ulimwenguni kote. Kwa miongo mingi hadithi hizi zilipotea na zilizokuwako zilikuwa fupi mno mara nyingi zikiwa mafupisho kwa ajili ya watoto. Halafu matoleo haya yamehifadhi vielelezo vya matoleo ya vitabu vya awali ambazo kwa hakika zinaongeza sifa za hadithi hizi ama kwa kutisha au kwa kuburudisha.
Kiswahili kina bahati ya kumpata mfasiri, Hassan Adam, Mtanzania mwenye ujuzi wa lugha zote tatu zilizohusika katika kutayarisha tafsiri hizi. Bwana Hassan Adam ni mkufunzi wa miaka mingi katika Taasisi ya Lugha za Kiafrika katika Chuo kikuu cha Cologne, Ujerumani.
|