Muhtasari
Mkuki na Nyota Publishers (MnNP) ni kampuni ya uchapishaji vitabu ya Tanzania iliyoanzishwa mwaka 1991, Dar Es salaam, Tanzania. Baada ya kuongoza Kampuni ya Uchapishaji Vitabu ya Tanzania Publishing House kwa muda wa miaka 18, Bwana Walter Bgoya alianzisha kampuni hii kwa lengo la kuchapisha vitabu vya taaluma ya juu – yaani kwa vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu ya juu. Katika kutilia mkazo zaidi uchapishaji wa vitabu vya aina hiyo, Mkuki na Nyota imeweza kuchapisha vitabu mbalimbali katika fani ya Sayansi ya Jamii, vikiwamo vitabu vya Sanaa, vitabu vya ziada kwa shule za msingi na sekondari na vitabu vya watoto wadogo.

Lengo
Lengo la Mkuki na Nyota ni kuchapisha vitabu muwafaka, vitabu nadhifu na vitabu vya bei nafuu kwa ajili ya masoko ya ndani na ya Kanda; na vitabu vya hali ya juu ya ushindani katika soko la kimataifa. Pamoja na vitabu vyake kuuzwa kwa kupitia maduka ya vitabu na vituo vingine, nchini na katika kanda ya Afrika, vitabu vya MnNP vinatafutiwa masoko na kuuzwa na wakala wake, African Books Collective (ABC) iliyoko Oxford, Uingereza. Kule marekani, Michigan State University Press ni washirika wa ABC katika kuwakilisha wachapishaji wanachama wa ABC.
ABC iliundwa kwa ushirika wa wachapishaji vitabu wa Afrika mwaka 1989, ili kuongeza mauzo ya vitabu vyao katika masoko ya nje. Bwana Walter Bgoya, Mkurugenzi Mkuu wa MnNP ni Mwenyekiti wa ABC.

Ingawa vitabu vyenye matumaini makubwa zaidi ya soko la nje ni vile vya taaluma ya juu, vitabu vingine vya kawaida, kwa mfano, makamusi ya Kiswahili na Kiingereza na vitabu vya watoto wadogo vinapendwa na kununuliwa hasa pale penye vyuo vikuu vyenye vitengo vya Masomo kuhusu Afrika na maktaba za umma.

Miradi Maalum
Vitabu vya Kiada
Licha ya kwamba ilipoanzishwa kampuni ya MnNP haikulenga sana katika uchapishaji wa vitabu vya shule, hata hivyo vitabu mbalimbali ilivyochapisha ilikuta vinachukuliwa na Wizara ya Elimu na Utamaduni kama vitabu vya ziada. Baadhi ya vitabu hivyo vimenunuliwa kwa makumi ya maelfu na vimefikia kupendwa sana na walimu na wanafunzi. Mifululizo kadhaa iko mbioni kutayarishwa na baadhi vimeshapitishwa na EMAC na vimeshaanza kutumiwa. Nia ni kuendelea kutayarisha na kuchapisha vitabu vya kiada kwa ngazi zote za elimu.

Sayansi ya Jamii
Pamoja na kuchapisha vitabu vingi vya taaluma ya juu katika fani hii vianvyotumiwa katika vyuo vikuu, MnNP imekuwa ikiwachapishia Economic and Social Foundation (ESRF), Research on Poverty Alleviation (REPOA), Research in Democracy in Tanzania (REDET), Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na UNICEF.

Timu ya Mkuki na Nyota
Kwa nyongeza ya uzoefu wa Bwana Bgoya wa miaka takribani 33 katika fani ya uchapishaji, kuna wafanya kazi wengine mahiri wa uhariri, utayarishaji na uundaji, utafutaji wa masoko na mauzo. Zaidi ya mafunzo kamilifu ya ndani, wafanya kazi wanatafutiwa na kupelekwa kwenye masomo kila inapowezekana na hadi sasa nafasi zimeshaptikana katika kampuni ya uchapishaji vitabu ya Chuo Kikuu cha Marekani kilicho Cairo na katika ofisi za ABC, Oxford kwa kujifunzia taaluma ya
Print on Demand.
Hawa wafanyakazi wa kudumu wanaungwa mkono na wengine wa kujiajiri, wakiwamo wahariri, wasanifu wa vitabu, na wasanii wa vielelezo vya vitabu. Kwa pamoja katika mwaka wa 2004 waliweza kutayarisha na kuchapisha jumla ya vitabu sitini (45 vya watoto na vingine 15 vikubwa) vya ubora wa hali ya juu ambayo ni sifa ya Mkuki na Nyota.